BODI YA FILAMU TANZANIA YAZITAKA KAMPUNI ZA FILAMU KUZINGATIA SHERIA NA KANUNI ZA FILAMU


 Katibu Bodi ya Filamu Tanzania, Bi. Joyce Fissoo akiongea na wahusijka wa Kampuni ya Kajala Entertainment wakati alipofanya nao mkutano leo ofisini kwake jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuwapa Sheria na Kanuni zilizokiukwa katika filamu ya Mbwa Mwitu.
 Mkurugenzi wa Kampuni ya Kajala Entertainment, Kajala Masanja akijitetea mbele ya Katibu wa Bodi ya Filamu Tanzania wakati aliitikia wito wa Ofisi ya Bodi hiyo leo jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuelezwa juu ya Sheria na Kanuni zilizokiukwa katika filamu yake ya Mbwa Mwitu.
 Mkurugenzi wa Kampuni ya Kajala Entertainment, Kajala Masanja akijitetea mbele ya Katibu wa Bodi ya Filamu Tanzania wakati aliitikia wito wa Ofisi ya Bodi hiyo leo jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuelezwa juu ya Sheria na Kanuni zilizokiukwa katika filamu yake ya Mbwa Mwitu.
 Meneja ambaye pia ni Mratibu wa Kampuni ya Kajala Entertainment, Bi. Leah Mwendamseke (kushoto) akitoa maelezo yake mbele ya Katibu wa Bodi ya Filamu Tanzania wakati aliitikia wito wa Ofisi ya Bodi hiyo leo jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuelezwa juu ya Sheria na Kanuni zilizokiukwa katika filamu ya Mbwa Mwitu.
 Mkurugenzi wa Kampuni ya Kajala Entertainment, Kajala Masanja akiweka sahihi ya kukubali kufanya marekebisho katika filamu yake pamoja na malipo ya faini mbele ya Katibu wa Bodi ya Filamu Tanzania wakati aliitikia wito wa Ofisi ya Bodi hiyo leo jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuelezwa juu ya Sheria na Kanuni zilizokiukwa katika filamu yake ya Mbwa Mwitu.
 Mkurugenzi wa Kampuni ya Kajala Entertainment, Kajala Masanja akiweka sahihi ya kukubali kufanya marekebisho katika filamu yake pamoja na malipo ya faini mbele ya Katibu wa Bodi ya Filamu Tanzania wakati aliitikia wito wa Ofisi ya Bodi hiyo leo jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuelezwa juu ya Sheria na Kanuni zilizokiukwa katika filamu yake ya Mbwa Mwitu.
 Katibu Bodi ya Filamu Tanzania, Bi. Joyce Fissoo akiweka sahihi yake katika fomu kuthibitisha makubaliano kati ya kampuni ya Kajala wakati alipofanya nao mkutano leo ofisini kwake jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuwapa Sheria na Kanuni zilizokiukwa katika filamu ya Mbwa Mwitu.
Katibu Bodi ya Filamu Tanzania, Bi. Joyce Fissoo akiagana na Mkurugenzi wa Kampuni ya Kajala Entertainment wakati alipofanya naye mkutano leo ofisini kwake jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuwapa Sheria na Kanuni zilizokiukwa katika filamu ya Mbwa Mwitu. PICHA ZOTE NA BENEDICT LIWENGA, MAELEZO-DSM
*********************************************
BODI ya Filamu Tanzania imezitaka Kampuni za filamu nchini kufuata Sheria na Kanuni mbalimbali wakati wa kutengeneza filamu ili kuepusha ukiukwaji wa Sheria na Kununi.
Rai hiyo imetolewa leo na Katibu wa Bodi hiyo, Bi Joyce Fissoo wakati alipofanya mkutano na Kampuni ya Kajala Entertainment ambapo mnamo Septemba 22, mwaka huu ilikagua Filamu fupi ya kampuni hiyo iliyopewa jina la Mbwa Mwitu yenye dakika 12 na kubaini baadhi ya makosa.

Akiongea wakati wa mkutano na wadau wa kampuni hiyo, Bi Fissoo alisema kuwa Bodi iliielekeza Kajala Entertainment kuifanyia marekebisho filamu hiyo katika dakika ya 7 ambapo ilionekana wanawake wakidhalilishwa na kubakwa kinyama na pia katika dakika ya 11 ambapo ilionyesha wizi na uvamizi.
Alisema kuwa, wahusika walielekezwa kufanya marekebisho hayo kwa kuondoa vipande husika na baada ya kufanya marekebisho hayo waliwasilisha Bodi ya Filamu nakala ya filamu iliyokuwa imefanyiwa marekebisho yenye dakika 12 na kupewa kibali namba 4261 ya tarehe 24 Septemba, 2014.

Bi Fisso aliongeza kuwa, mnamo tarehe 25 Septemba, 2014 katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam, filamu hiyo fupi ilionyeshwa bila ya kuzingatia marekebisho yaliyokuwa yameelekezwa kwa mujibu wa Sheria kwa kuzingatia kifungu cha Sheria cha 19 (2) (a).
“Baada ya ukiukwaji wa Sheria katika kifungu cha 19 (2) (a) na kile cha 24 (i), (m) na (n) vya Kanuni za Sheria ya Filamu husika, wahusika waliitwa mara mbili kufika Bodi ya Filamu lakini hawakufanya hivyo, lakini baada ya kumbushio na kalipio wahusika baadaye walifika Ofisi za Bodi katika kikao cha tarehe 13 Novemba mwaka huu”, alisema Bi. Fissoo.
Alieleza kwamba, wahusika walikiri kuwa walipata ujumbe wa wito wao wa kuitwa na Bodi hiyo ambapo Mratibu wa masuala yote ya Kampuni ya Kajala Entertainment, Bi. Leah Mwendamseke aliieleza Bodi kuwa anaomba asamehewe kwa kuwa walikuwa na shughuli nyingine mbalimbali.
Naye Mkurugenzi wa Kampuni hiyo, Kajala Massanja aliiomba radhi Bodi ya Filamu Tanzania huku akisema kuwa mara nyingi yeye huwa amekuwa akiwaachia wsaidizi wake kutekeleza majukumu ya kampuni yake ingawa yeye kama mmiliki wa kampuni hiyo anawajibika moja kwa moja.
Aidha, Bodi iliitaka Kajala Entertainment kueleza sababu ya kukiuka maelekezo ya Bodi ambayo yalikuwa kwa mujibu wa Sheria na Kanuni zake licha ya mtunzi na mwandishi wa musuada na muongozaji wa filamu hiyo, Bi. Leah Mwendamseke alijitetea kuwa alifanya utafiti na kukutanana vijana mbalimbali waliowahi kujihusisha na vitendo vya uhalifu.

Hata hivyo, Leah Mwendamseke alishindwa kuoanisha uhalisia wa matokeo ya utafiti wake na ujenzi wa visa vya hadithi ya filamu ambayo inaweza kupeleka ujumbe chanya kwa jamii, huku wahusika wakieleza kwamba lengo lao kubwa lilikuwa ni kuelimisha jamii kuhusu maovu yanayotokea na namna ya kuyaepuka ambapo mtunzi huyo aliahidi kurekebisha vipengelee husika katika filamu hiyo ili kuwa na filamu bora.
Kwa upande wake Mwakilishi toka Ofisi ya Makao Makuu ya Polisi Tanzania, Sylivester Mganga aliushauri uongozi wa Kajala Entertainment kufuata maelekezo na kuzijua Sheria mbalimbali zinazohusu mambo ya filamu kwa kuvishirikisha vyombo vya ulinzi na usalama kabla ya kujichukulia maamuzi ya kutengeneza filamu zenye kutishia amani ya nchi.
Bodi ya Filamu Tanzania imetoa onyo kali kwa wahusika kwa kutengeenza filamu zenye kuonyesha ama kukuza uhalifu na udhalilishaji bila kuainisha mkondo wa Sheria licha ya msamaha kutokana na kosa hilo ambapo Bodi hiyo imeitaka kampuni hiyo ilipe faini ya shilingi milioni moja kwa mujibu wa kifungu cha 47 (2) (a) cha Kanuni za Sheria ya Filamu ambayo wahusika waliridhia adhabu hiyo.