Mwenyekiti wa Bodi wa Busara Promotions,
wandaaji wa tamasha la Sauti za Busara, Simai Mohammed (katikati)
akiongea na wandishi wa habari (Hawapo pichani) wakati wa mkutano wa
wanahabari Jijini Dar es Salaam, juu ya tamasha la 12 la Sauti za
Busara, litakalofanyika, Februari 12 hadi 15, mwaka huu, Ngome Kongwe,
Zanzibar. Wengine (kushoto) ni Meneja wa tamasha hilo, Journey
Ramadhani. na upande wa kulia ni Mkurugenzi wa tamasha hilo, Yusuf
Mahmoud ‘Dj Yusuf, akifuatiwa na msanii wa bongo fleva nchini, Ali Kiba
(kulia).
Msanii wa Bongo
fleva nchini, Ali Kiba akiimba akapela moja ya nyimbo zake wakati wa
mkutano huo na wandishi wa habari (Hawapo pichani), katika mkutano huo
juu ya ushiriki wake kwenye tamasha hilo linalotarajia kufanyika
Februari 12 hadi 15, Ngome Kongwe, Zanzibar. kushoto kwake, ni
Mkurugenzi wa tamasha hilo, Yusuf Mahmoud ‘Dj Yusuf, akifuatiwa na Mwenyekiti wa Bodi wa Busara Promotions, Simai Mohammed.
Simai, Dj Yusuf na Kiba wakiwa
wameunganisha mikono kwa kusalimiana ikiwa ni ishara ya Umoja na Amani,
kama Kauli mbiu ya mwaka huu ya tamasha hilo inavyohimiza amani.
Ali Kiba katika ‘Selfie’ na Mwenyekiti wa
Bodi ya Busara Promotions, Simai Mohammed, muda mfupi baada ya
utambulisho wa msanii huyo juu ya kupiga shoo kwenye tamasha la 12 la
Sauti za Busara, litakalofanyika Februari 12 hadi 15, Zanzibar.
Na Andrew Chale
Mkali wa muziki
wa kizazi kipya nchini, Ali Kiba ametamba kukonga nyoyo watu mbalimbali
watakaojitokeza kwenye tamasha la 12 la Sauti za Busara linalotarajia
kufanyika, Februari 12 hadi 15, Ngome Kongwe, Zanzubar.
Ali Kiba alieleza hayo leo
Alhamisi, Januari 29. wakati wa mkutano wa ulioandaliwa na Busara
Promotions, wandaaji wa tamasha hilo kubwa la Kimataifa linalofanya
muziki wa ‘Live’, ambapo kwa mwaka huu zaidi ya wanamuziki na vikundi
37, watatoa burudani kwenye tamasha hilo kwenye viunga vya Ngome Kongwe,
Unguja, Zanzibar.
Akizungumza
mbele ya wandishi wa habari, Ali Kiba alisema kwa sasa amejiandaa kutoa
burudani ya aina na ambayo itakonga nyoyo kwa watu wote watakaojitokeza
kushuhudia tamasha hilo.
“Hii itakuwa ni
zawadi kwa watanzania wote kunishuhudia nikiimba ‘live’ bila kutumia
‘cd’ kama wafanyavyo wengine. Mimi ni mwanamuziki na nimesoma muziki
hivyo nitapiga muziki wa nguvu jukwaani” alisema Ali Kiba.
Na kuongeza kuwa,
kwa sasa yupo kwenye mazoezi ya muda mrefu wa kujifua na bendi maalum
kwa ajili ya shoo hiyo huku akitamba kuwa, yeye ni msanii kwani muziki
aliusomea na kujifunza huko nyuma alipokuwa katika Nyumba ya kuibua
vipaji THT, ambapo alijifunza vitu vingi ikiwemo kuimba muziki wa bendi
na ‘live’.
Aidha, aliwaomba wapenzi na wadau wa muziki kujitokeza kwa wingi
kushuhudia tamasha hilo kwani wasanii mbalimbali wa ndani na nje watatoa burudani ya kipekee.
Kwa upande wake,
Mwenyekiti wa bodi ya Busara Promotion, wandaaji wa tamasha hilo, Simai
Mohammed, alisema tamasha limeweza kuongeza ajira na uchumi wa Zanzibar
kwani pia limeongeza fursa za utalii.
Kwa upande wake,
Meneja wa tamasha hilo, Journey Ramadhani, alisema tamasha hilo
limeweza kuongeza fursa kila mwaka ikiwemo kutoa ajira kwa vijana wa
kitanzania kwa asilimia 90, ambapo kwa mwaka huu wanatarajia kuwa na
watendaji kazi na wa kujitolewa watakolipwa katika kusaidia tamasha
hilo, zaidi ya watu 150.
Kwa upande wake,
Mkurugenzi Mkuu wa tamasha hilo, Yusuf Mahmoud ‘Dj Yusuf’ alisema
tamasha hilo limeweza kuibua wasanii mbalimbali ikiwemo kujitangaza
kimataifa.
Aidha, Dj Yusuf
alieleza kuwa, tamasha la mwaka huu litaendana na kauli mbiu ya kuimiza
Amani, pia wameandaa tuzo maalum na zawadi maalum kwa wasanii wa
Tanzania watakaoshinda katika kutunga nyimbo za amani.
Mbali na Ali
Kiba, Wasanii wengine Isabel Novella kutoka Msumbiji, Ihhashi
Elimhlophe (Afrika Kusini), Tcheka (Cape Verde), Diabel Cissokho
(Senegal), Culture Musical Club (Zanzibar), Msafiri Zawose (Tanzania),
Aline Frazão (Angola), Tsiliva (Madagascar), Leo Mkanyia and the
Swahili Blues Band (Tanzania), Mohamed Ilyas & Nyota Zameremeta
(Zanzibar), Thaïs Diarra (Senegal / Mali / Uswisi), Liza Kamikazi
and band (Rwanda), Erik Aliana (Cameroon), Mpamanga (Madagascar),
Mgodro Group (Zanzibar), Rico Single & Swahili Vibes (Zanzibar),
Zee Town Sojaz (Zanzibar), Ifa Band (Tanzania) na wengine wengi.
Maelezo zaidi yanapatikana katika www.busaramusic.org