Wanaume mnajua hili: Mfanyie mwanamke mautundu haya akuzidishie raha


MAMBO vipi ndugu zangu? Ni furaha yangu kwa mara nyingine tena kukutana nanyi wapendwa wasomaji wa safu yetu hii. Tumshukuru Muumba wetu kwa kutujaalia uhai na afya njema, lakini zaidi ya hapo tumshukuru pia kwa kutuumbia kitu mapenzi au siyo jamani?
Siku zote hatutaacha kuzungumza juu ya mapenzi kwani ni ukweli usiopingika kwamba mapenzi ndiyo maisha yetu.
Tunafanya kazi usiku na mchana, tunahangaika huku na huko, lakini mwisho wa siku tunafikiria jinsi gani tutapata kuboresha na kufurahia maisha na wapenzi wetu.
Tunafikiria pia ni jinsi gani tunaweza tukapata utulivu na amani katika maisha ya kimapenzi na wapenzi wetu, waume zetu au wake zetu katika siku zote za maisha yetu.
Ndugu zangu, Mungu ametuwekea mapenzi ili tupate raha na amani katika maisha yetu.
Kwa maana hiyo, wale wanaoyachezea na kuyavuruga mapenzi kwa makusudi kwa kuumiza hisia za wenzao kisha kuwasababishia vilio si watu wa kupendeza mbele ya macho ya wale wanaojua hasa nini maana ya mapenzi.
Wanawake ni watu wa kuheshimika na kupewa furaha wanayohitaji. Unapompata mwanamke anayekupenda na kukuheshimu, huna sababu ya kumfanya ajute kuwa na wewe.
MPENDE NA MTHAMINI!
Yawapasa wanaume mfahamu kuwa, wanawake ni zawadi kwenu, pumziko na tulizo la mioyo yenu. Wanawake ndiyo raha na amani kubwa ya maisha yenu.
Kosa kubwa mnalofanya wanaume ni kuutumia vibaya mfumo dume hasa katika suala nyeti kama mapenzi.  Mapenzi si ubabe, mapenzi ni upole na ukarimu.
 Pamoja na kwamba mmebarikiwa kwa kupewa nafasi ya kuwa kichwa katika nyumba lakini linapokuja suala la kurekebisha tofauti zinazojitokeza katika uhusiano wenu, si vyema kutumia njia za kibabe.
Niwaambie kitu, wanawake ni wa hisia zaidi na waliobarikiwa kuwa na upendo wa hali ya juu na ndiyo maana wakapewa dhamana ya kubeba mtoto tumboni kwa miezi tisa na pia kumnyonyesha na kumlea kwa miaka kadhaa, wewe mwanaume ungeweza?
Nasema ni watu wa hisia kwa sababu, hivi uliwahi kufikiri ni kwa nini wanawake huridhika na kujisikia poa kweli wanapopewa zawadi kama ya maua na kadi zenye ujumbe wa mapenzi ukilinganisha na wanaume?
Unafikiri ni kwa nini wana machozi ya haraka wanapotendwa? Au unafikiri ni kwa nini wanapenda kutumiwa ‘love sms’ zaidi kuliko kupigiwa simu? Jiulize.
Mimi nawaona wanawake kama watu wa kuheshimiwa na kupendwa kwa dhati.  Mkumbuke wanawake ndiyo mama zetu, walezi wetu na ndiyo nyumba zetu. Jaribuni pia kujicontroo na huo mnaouita ukijogoo kwamba eti ninyi ni watu msioridhika na mpenzi mmoja.
Jaribuni kufanya kila mnaloweza kuifuta ile dhana ya kwamba wanaume hawaaminiki hata kidogo. Ridhika na mpenzi uliyenaye, heshimu hisia zake na thamini mapenzi yake kwako na mpe ile kitu roho inapenda!
Ni hayo tu kwa leo.