Msimu wa utoaji tuzo kwa wasanii wa muziki Tanzania wanaofanya vizuri umewadia huku mchakato wa awali wa mchanganuo wa tuzo hizo za Kili Tanzania Music Awards 2015 (KTMA) ukianza rasmi wiki hii.
Wakati mchakato huo ukisubiri mashabiki kuamua msanii yupi aingie katika kipengele kipi, wasanii wengi watakuwa matumbo joto kwa kile kinachoelezwa kwamba KTMA sasa zimekubalika zaidi kwao na mashabiki wa muziki.
Hata hivyo, msimu huo unatojawa kuwa wenye neema kwa wasanii, unazua maswali mengi vichwani mwa wasanii na mashabiki wao moja likiwa; ni nani atavunja rekodi iliyowekwa na mwanamuziki Diamond Platnumz mwaka jana?
Mbali na Diamond kuvunja rekodi msimu uliopita, Bendi ya muziki wa dansi ya Mashujaa pia iliwahi kunyakua tuzo tano mwaka 2013, huku wasanii, Kala Jeremiah na Ommy Dimpoz wakinyakua tuzo tatu kila mmoja.
Shabiki wa muziki wa kizazi kipya na mfanyabiashara katika Soko la Kariakoo, Omary Shaban alisema ushindani kwa mwaka huu utakuwa mkubwa kwa tuzo hizo, hasa ikizingatiwa uwepo wa wanamuziki wengi wazuri waliofanya kazi tofauti, zenye ubora na viwango vya juu.
“Mwaka jana Diamond Platnumz alinyakua tuzo nyingi kwa kuwa alijaribu kufanya kitu tofauti, lakini alichokifanya na wengine wamefanya. Hivyo, ana ushindani mkubwa, pia Alikiba ambaye alikuwa kimya amerudi. Hawa wawili ni washindani wakubwa, hivyo video zao zitalumbana sana, yaani tunasubiri kumjua mkali nani,” anasema Shaban.
Mshabiki mwingine, Ally Elly wa Dar es Salaam alisema ni vyema kusiwepo ubabaishaji ili wapatikane washindani na washindi halisi wa tuzo hizo kwa mwaka huu.
Mchakato utakavyokuwa
Waandaji wa mashindani hayo walisema kuwa kwa mwaka huu kuna ongezeko la baadhi ya mambo, lengo likiwa ni kuboresha utoaji wa tuzo hizo na kuwapa fursa Watanzania kupendekeza wasanii watakaowania tuzo hizo kwa kuwapigia kura waingie kwenye kinyang’anyiro kwa njia tatu kuu.
“Tumekuwa na juhudi za makusudi za kutenga fungu kubwa na kuongeza ushiriki wa wataalamu kwenye fani husika ili kuziendeleza, kuzikuza na kuziongezea thamani na umaarufu wa tuzo hizi kimataifa mwaka hadi mwaka,” alisema Meneja wa Bia ya Kilimanjaro, Pamela Kikuli. Bia hiyo ndiyo wadhamini wakuu wa tuzo hizo
“Wananchi watapata fursa ya kupiga kura kupendekeza wasanii katika vipengele mbalimbali kwa kutumia njia tatu; kwa mfumo wa website ya www.ktma.co.tz, mfumo wa mtandao wa WhatsApp na kwa njia ya SMS.” Alisema katika WhatsApp, mpigakura ataweza kutumia namba ya simu na SMS kwa kutuma ujumbe wa neno KTMA au KILI na kisha kufuata maelekezo kwa ajili ya kukamilisha zoezi hilo litakaloanza rasmi Machi 30 hadi Aprili 19, mwaka huu litakapositishwa.