GARI LA KANUMBA LAGOMA KUTOKA SOKONI


Gari la Kanumba Lashindwa Kuuzika Sokoni
Ikiwa ni miaka mitatu sasa imepita tangu aliekuwa staa wa Bongo  Movies, marehemu Steven Kanumba, inadaiwa kuwa gari alilokuwa akilitembelea aina ya Toyota Lexus lenye namba za usajili T750 AER limezidi kudoda sokoni.
Kwa mujibu wa chanzo makini cha gazeti la Risasi kimepenyeza habari kuwa gari hilo lililonunuliwa na marehemu kwa shilingi milioni 78, linapatikana maeneo ya Msasani, jijini Dar kwenye jengo la mikopo ambapo linauzwa kwa bei chee ya shilingi milioni 18 hadi 14.
“Nilikuwa nikijipitia kukagua magari lakini ghafla nikakutana na gari la Kanumba. Sikuamini mpaka pale nilipoingia na kulipiga picha kisha nikaambiwa na thamani yake,” kilisema chanzo.Chanzo kiliendelea kutiririka kuwa huenda kuna mkopo ulichukuliwa na kuacha dokumenti zote za gari hiyo na iliposhindikana kulipwa gari hiyo ikapigwa mnada.
“Sidhani kama gari kali kama ile ipigwe bei ya milioni 18 tu, lazima kutakuwa na mkopo ambao haujamalizwa ndiyo maana limepigwa kiasi hicho cha pesa ili kukamilisha.”Awali ilisemekana kuwa gari hilo lilikabidhiwa kwa msanii wa filamu Bongo, Mahsein Awadh ‘Dk. Cheni’ ili alinunue kwa gharama ya shilingi milioni 40 lakini kwa kuwa liligundulika na matatizo mengi akawa tayari kutoa shilingi milioni 25 ambapo pia ilishindikana na kurudishwa kwa familia ya Kanumba.
Gazeti hilo lilimtafuta mama Kanumba, Flora Mtegoa ili kujua anazungumziaje gari hilo kudoda sokoni, alijibu:“Mimi sijui chochote kuhusu hilo gari naona mnazidi kuniumiza tu hapa naumwa, hata kama nimeuza au limefanywaje jamani maswali mengine yanaumiza hebu niacheni maana sijui kinachoendelea kuhusu hilo gari,” alisema Mama Kanumba.

0 Response to "GARI LA KANUMBA LAGOMA KUTOKA SOKONI"

Chapisha Maoni